Kadinali wa Kanisa la Katoliki nchini John Njue amewahimiza Wakenya kuishi kwa amani na upendo msimu huu wanapojiandaa kusherehekea mwaka mpya.
Akizungumza wakati wa misaa wa kuidhinishwa kwa askofu wa kanisa la katoliko dayosesi ya Mombasa Martin Kivuva siku ya jumanne, Njue, alisema umoja na utangamano ndicho kitu ambacho kitasaidia kuleta uwiano baina ya Wakenya.
"Amani na uwiano tutapata tu iwapo sisi wenyewe tutakumbatiana, kuja pamoja na kuweka kando tofauti zetu na kupendana," alisema Njue.
Kiongozi huyo, pia aliwahimiza Wakenya kutokubali kugawanywa kwa msingi wa kisiasa wala kidini huku akitoa mfano wa wanawake waumini wa dini ya Kiislamu walivyosimama na wenzao wakristo hivi majuzi basi walimokuwa wakisafiria lilipotekwa nyara na wanamgambo wa Al Shabaab.
"Juzi mliona wenzetu waislamu walivyosimama na wanakristo na kuwaokoa mikononi mwa magaidi, huo ndio mfano tunaofaa kuufuata," akaongeza.
Kwa upande wake askofu Martin Kivuva, aliapa kutekeleza waajibu wake kama mtumishi wa Mungu huku akiwataka Wakenya kuheshimiana na kusaidiana bila kuangalia tabaka la mtu.