Share news tips with us here at Hivisasa

Serikali ya Denmark imetoa ufadhili wa shilingi bilioni 15 kwa serikali ya Kenya kushughulikia miundo msingi katika bandari ya Mombasa ili kuimarisha biashara baina ya mataifa hayo mawili.

Waziri wa maswala ya kigeni wa Denmark Kristian Jensen amesema kwamba ufadhili huo unatarajiwa kufanikisha malengo ya ruwaza wa mwaka wa 2030 ikiwemo kuimarisha uchukuzi, mazingira bora ya afya, ajira na ukuaji wa uchumi pamoja na usimamizi bora katika bandari ya Mombasa.

Akiongea na wanahabari baada ya kukagua miradi mbali mbali iliyotekelezwa katika bandari hiyo kupitia ufadhili huo, Jensen alisema kwamba ushirikiano baina ya mataifa hayo mawili utazidishwa ili kuimarisha biashara, uwekezaji na uchumi.

"Tunahakikisha tunashirikiana vyema na taifa la Kenya katika kuimarisha biashara na kukuza uchumi, na tutaendelea kufadhili ili kuona kwamba bandari ya Mombasa inafanya vyema katika shughuli za kibiashara na kusaidia jamii," alisema Jensen.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Halmashauri ya Bandari nchini Gichiri Ndua, ushirikiano huo umesaidia pakubwa katika upanuzi wa barabara kutoka barabara ya Moi Avenue kupitia kona ya Mtongwe hadi lango kuu la KPA, pamoja na upanuzi wa eneo la kuegesha meli la tano katika bandari hiyo.

Naye mkurungezi wa Shirika la kibiashara la Afrika mashariki David Stanton amesema kwamba juhudi hizo zitaleta mshikamano wa kibiashara na kuboresha sekta ya biashara, uchukuzi na miundo msingi nchini.

Uhusiano wa kibiashara baina ya taifa la Denmark na Kenya umedumu tangu taifa hili kujipatia Uhuru, na juhudi hizo zinaendelezwa kufuatia demokrasia na ukuzaji uchumi.