Kulishuhudiwa kisanga Alhamisi asubuhi katika kijiji cha Eburru huko Gilgil, baada ya wakazi kufanya maandamano kutokana na barabara mbovu za eneo hilo.
Wakazi hao wamesema kuwa wamesahaulika kwa muda mrefu na viongozi wao, akiwemo gavana, tukio ambalo limewaacha wakitaabika.
Kulingana nao, barabara za eneo hilo zimekuwa hazipitiki kwa mda mrefu sasa, na haswa wakati huu wa mvua, na wameilaumu serikali ya kaunti ya Nakuru na hazina ya CDF ya Gilgil kwa kukosa kushughulikia masaibu yao.
Kiongozi mmoja kwa jina Lydia Nyota amesema kuwa licha ya kupata usaidizi kutoka kwa kampuni zinazopakana na kijiji hicho, hakuna kitu serikali imewafanyia hadi kufikia sasa.
“Wengi wanaadhirika kwa sasa na mvua inayoendelea kunyesha inaendelea kusababisha maafa makubwa na kuharibu barabara hiyo hata zaidi, tunataka hatua ya dharura kuchukuliwa ili kukarabati barabara hii,” Nyota alisema.
Naye Peter Mbugua aliongeza kuwa eneo hilo hukuza megawati tano ya kawi ya mvuke, na linafaa kushughulikiwa kama maeneo mengine nchini.