Share news tips with us here at Hivisasa

Wanawake wawili waliokuwa wakitoka kwenye shughuli ya mazishi waliaga dunia baada ya gari walilokuwa wakisafiria kuhusika kwenye ajali mbaya katika barabara ya Naiobi kuelekea Nakuru.

Wengine wawili wameachwa wakiuguza majeraha kufuatia mkasa huo wa Jumapili jioni karibu na kituo cha kufanyia biashara cha Matches kwenye barabara hiyo.

Mmoja wa walioshuhudia Abel Kimathi amesema kuwa gari walimokuwa wawili hao lilipoteza mwelekeo na kugongana na basi moja lililokuwa likielekea mjini Nairobi.

“Wote hao walikuwa kwenye gari moja na walikuwa wakitoka hafla ya mazishi ya rafiki yao mjini Kisumu wakati ajali hiyo ilitokea.” Kimathi aliongeza.

Kwingineko, abiria kadhaa wamepata majeraha mapema Jumatatu baada ya gari la aina ya Nissan walilokuwa wakisafiria kugongana na lingine la kubeba mizigo karibu na eneo la Ihindu kwenye barabara hiyo.

Matatu hiyo iligonga gari hilo upande wa nyuma na kuanguka huku abiria sita kati yao wakipata majeraha mabaya na kukimbizwa katika hospitali kuu ya wilaya ya Naivasha.