Serikali ya kaunti ya Lamu imeishtumu tume ya Kitaifa ya Ardhi nchini kwa madai kuwa inalenga kupeana kiasi kikubwa cha ardhi kwa serikali katika maeneo ya Kililara bila ya kuwahusisha viongozi wa kaunti hiyo.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Gavana wa kaunti ya Lamu Isaah Timamy amesema kuwa Tume hiyo iliyo chini ya mwenyekiti wao Daktari Mohammed Swazuri inataka kupeana ardhi ili kufanikisha mradi wa ujenzi wa bandari mpya ya Lamu iliyo chini ya mradi wa Lapset, hatua ambayo Gavana Timamy anasema kuwa imekiuka sheria za ugatuzi.

Akizungumza na wanahabari siku ya Alhamisi, Timamy amemtaka Swazuri kufuata utaratibu unaofaa katika kupeana ardhi hiyo huku akipuuzilia mbali malengo ya tume hiyo akisema kuwa inalengo kuwahujumu wananchi.

"Swazuri ana njama mbaya ya kuwakandamiza wakaazi wa Lamu kwani hekari anazolenga kuchukua na kuipa serikali ni nyingi mno zaidi ya hekari elfu 70 katika maeneo ya Kililara, hiyo kama viongozi hatutakubali na lazima tuhusishwe katika mazungumzo na tujue vile wakaazi wetu watakavyolipwa fidia," alisema Timamy.

Timamy aidha amesema kuwa swala hilo lazima wakaazi na viongozi wa kaunti hiyo kuhusishwa katika mazungumzo na kueleza bayana jinsi wakaazi watakavyofidiwa kabla ya mradi huo kuanza, la sivyo viongozi wa kaunti hiyo watapinga swala hilo.

Tume ya Kitaifa ya ardhi nchini imependekeza kupeana ardhi ya hekari elfu 70 ya maeneo ya Kililara kwa serikali kutumika katika ujenzi wa Lapset katika kaunti ya Lamu.