Onyo kali imetolewa kwa walimu wakuu katika shule za upili za umma watakaopatikana wakitoza wazazi karo kupita kiasi kilichoidhinishwa na serikali.
Akizungumza na mwandhishi huyu siku ya Alhamisi, afisaa katika shirika la Elimu Yetu Coalition linalopigania haki ya elimu ya wanafunzi hapa nchini, Catherine Asego, alisema kulingana na sheria ya elimu ya msingi ya mwaka wa 2013, ni kinyume cha cheria kwa mwalimu mkuu yeyote kutoza karo zaidi.
Aidha, Asego alisema kuwa jopo lililotwikwa wajibu wa kuainisha kiwango cha karo mnamo Agosti 26, 2014, lilipendekeza karo ya shule za mabweni za umma kuwa shilingi elfu 66,424, serikali ikilipa shilingi elfu 12,870, huku wazazi wakitakiwa kulipia shilingi elfu 53, 554 pekee.
katika shule za kutwa, karo ni shilingi elfu 22,244, serikali ikilipa shilingi elfu 12,870 huku wazazi wakilipia shilingi elfu 9,374 pekee.
Asego alisema kuwa katika shule zenye mahitaji spesheli, karo ni shilingi elfu 69,810, serikali ikilipa shilingi elfu 32,600, huku wazazi wakilipia shilingi elfu 37,210 pekee.
Asego amewataka wakuu wa elimu katika wilaya kuhakikisha wanatekeleza agizo la sheria lililopitishwa ili wanafunzu humu nchini wasinyimwe haki yao ya kupata elimu bora.
Vilevile, afisaa huyo ametoa wito kwa vyombo vya habari kuhakikisha wanaangazia jambo hilo ili kuwafichua walimu wakuu ambao wanaendelea kuwadhulumu wazazi kwa kuwatoza karo za juu.
Mapendekezo hayo yalianza kutekelezwa Januari 5, 2015, huku kukiwa na madai kwamba kuna baadhi ya walimu wakuu ambao wanaendelea kukiuka mwongozo huo.