Share news tips with us here at Hivisasa

Wakazi wa kaunti ya Nyamira wamepata sababu ya kutabasamu baada ya serikali ya kaunti hiyo kupata ufadhili wa mashine mbalimbali za kima cha shillingi millioni 50 zitakazosambazwa kwenye hospitali na zahanati zote katika kaunti hiyo. 

Akihutubu wakati wa kupokea ufadhili huo wa serikali ya Ujerumani siku ya Jumatano Gavana Nyagarama aliwahimiza wahudumu wa afya kuhakikisha mashine hizo zinatumika vizuri. 

"Tumepokea mashine za kurahisisha kazi kwa wahudumu wa afya kwenye hospitali zetu, na ili kuhakikisha kuwa tumefanikiwa kuwahudumia vyema wakazi wa kaunti hii sharti wahudumu wajitolee kuhakikisha kuwa wanatumia vizuri mashine hizi," alisema Nyagarama. 

Gavana Nyagarama aidha aliongeza kwa kusema kuwa mashine za radiographa zilizoekezwa kwenye hospitali ndogo ya Nyansiongo na Nyamusi zitaanza kutumika chini ya miezi miwili ijayo. 

"Serikali yangu imo mbioni kuhakikisha huduma za afya ziko karibu na wananchi ndio maana tumewekeza pakubwa kwenye sekta ya afya na mashine za radiographa tulizoezeka kwenye hospitali ndogo ya Nyansiongo na Nyamusi zitaanza kuwahudumia wakazi wa maeneo hayo hivi karibuni," aliongezea Nyagarama.