Serikali ya Kaunti ya Kisii imeombwa kutoa usaidizi kwa wakulima wa majani chai ili kuwaepusha kupata hasara.
Kulingana na wakulima wa majani chai katika kaunti hiyo ya Kisii bei ya mbolea ya majani chai ambayo wanakabidhiwa kutoka halmashauri ya KTDA ni ya juu mno ikilinganishwa na ya hapo awali.
Wakizungumza na waandishi wa habari siku ya Alhamisi mjini Marani, wakulima hao wakiongozwa na Cyrus Ombati walisema bei ya mbolea wanayoletewa kutoka halmashauri hiyo ni ya juu mno.
Wakulima hao waliomba serikali ya Kaunti ya Kisii kuwapunguzia bei hiyo ambayo walisema imeongezeka katika siku za hivi maajuzi.
Wakulima hao waliiomba serikali ya kaunti kupitia mkuu wa idara ya kilimo katika Kaunti ya Kisii Vincent Sagwe, kuingilia kati na kuwapa suluhu la haraka.
Pia walimwomba Gavana James Ongwae kufuatilia suala hilo na kubaini kwa nini bei ya mbolea huongezwa kila mara.
“Tunaomba gavana wetu kuyasikia malalamishi yetu na kufuatilia swala hili ili aweze kubaini kwa nini tunaongezewa bei ya mbolea ilihali pesa tunapata pesa kidogo tunapouza mazao yetu,” alisema Ombati.
Aliongeza, “Bei ya mbolea imepandishwa kutoka shilling 1,950 hadi shillingi 2,700 kwa kila mfuko wa kilo 50 na tunaomba serikali ya kaunti itupunguzie bei hiyo.”