Mwanamke moja wa umri wa makamu anazuiliwa na maafisa wa polisi katika kituo cha Inuka baada ya kumchapa mwanawe wa kike wa umri wa 9 hadi akafariki katika eneo la Likoni usiku wa kumkia Alhamisi, Machi 17, 2016.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akithibitisha kisa hicho, afisa mkuu wa polisi eneo la Likoni Willy Simba amesema kuwa mwanamke huyo kwa jina Mercy Afandi Likanya alimchapa mwanawe hadi akazirai baada ya ugomvi wa kinyumbani na mumewe.

Simba amesema kuwa mtoto huyo wa kike wa shule ya msingi ya Tulia Moyo alipatikana na majeruhi mabaya kichwani baada ya kufikishwa katika hospitali kuu ya ukanda wa Pwani na kuthibitishwa kuaga dunia.

"Tukio limetokea usiku katika eneo la Inuka hapa Likoni ni tukio la kuhuzunisha kuona mama akiuchapa mtoto wake mpaka kumpa majeruhi mabaya ya kichwa na kuripotiwa kufariki hiyo lazima hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi ya huyo mwanamke kwani hiyo ni kunyanyasa mtoto mdogo," alisema Simba  wakati akizungumza na wanahabari katika eneo la Likoni siku ya Alhamisi.

Maafisa wa polisi wameanzisha uchunguzi kuhusiana na kisa hicho huku mwili wa mwendazake ukihifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti katika hospitali kuu ya ukanda wa Pwani.

Hata hivyo mwanamke huyo anasubiri kufikishwa mahakamani baada ya kukamilika kwa uchunguzi huku afisa mkuu wa polisi eneo hilo akitoa onyo kwa wakaazi dhidi ya kuwanyanyasa watoto wadogo.