Kanisa sasa limetaka kujumuishwa kwenye mpango wa kuwapa wakongwe pesa ili wote waweze kunufaika.
Haya yamejiri huku ripoti zikiibuka kuwa ni wakongwe wachache tu ambao hufaidika na mpango huo wa kuwawezesha kukijikimu kimaisha, miaka kadhaa tangia kubuniwa kwa mfumo huo. Mpango huo maarufu hujulikana kama Cash Transfer Program.
Kulingana na Pasta Mary Mwihaki wa kanisa la Prayers Faith International, wakati umefika ambapo serikali inafaa kushirikisha kanisa katika baadhi ya miradi inayohusu ‘Wanjiku’ moja kwa moja.
Mhubiri huyo alisema hayo baada ya washirika wa kanisa hilo kuzuru kitongoji duni cha Mithuri mjini Naivasha ambapo walitoa zawadi za chakula, nguo na vifaa vingine kwa wakongwe wanaoishi peke yao.
Kiongozi huyo wa dini alisisitiza hiyo ni moja wapo ya mikakati walioweka kuwapa wakongwe maisha bora kama Wakenya wengine.
“Kanisa lina uwezo wa kutambua kwa haraka wakongwe na jamii zenye mahitaji. Kwa hivyo kama serikali inataka uwazi kwenye suala hili la kuwawezesha wakongwe, haina budi ila kushirikisha kanisa,” alisema Mwihaki.
Mmoja wa wakongwe walionufaika Nyambura Gitare mwenye umri wa miaka 85 amesema kuwa hawapati pesa hizo na hata hawajui jinsi ya kujiandikisha.