Share news tips with us here at Hivisasa

Mkurugenzi wa Elimu katika Kaunti ya Nakuru Esther Muiru amesema kuwa serikali inaendesha misako ya dharura dhidi ya shule mbalimbali mjini Nakuru, kuhakikisha kuwa masomo ya ziada hayaendelezwi na kuwa wazazi hawalazimishwi kulipia masomo hayo.

Akizungumza katika mahojiano ofisini mwake na mwandishi huyu siku ya Jumatano, Muiru alitoa onyo kwa shule zinazowalazimu wanafunzi kulipa pesa ili waweze kupata masomo ya ziada, kwa kusema kuwa shughuli hiyo ni kinyume cha sheria.

Hata hivyo, alisema kuwa Wizara ya Elimu haijapinga masomo ya kujirekebisha yanayoendelezwa shuleni, na kufafanua kuwa kile ambacho kimepigwa marufuku ni masomo ya ziada, ambapo wazazi na wanafunzi hulazimishwa kulipia masomo hayo.

Licha ya hayo, alisema endapo wazazi wa shule wataamua kuwapa walimu kiwango fulani cha fedha kama ishara ya kuwashukuru au kuwatia moyo baada yao kuendeleza masomo hayo ya kujirekebisha , basi ofisi yake haiwezi kuwashutumu walimu hao.

Wakati huo huo, Bi Muiru alikashifu mbinu zinazotumiwa na walimu kuwalazimu wanafunzi kuhudhuria masomo ya ziada yanayotozwa fedha kama vile kuwaagiza wanafunzi kufika shuleni wakiwa wamevalia mavazi ya nyumbani wakati wa likizo, au kufanya shughuli hiyo katika majumba yaliyojificha.

Alisisitiza kuwa masomo ya ziada yalipigwa marufuku mwaka wa 2008 na aliyekuwa Waziri wa Elimu Profesa Sam Ongeri, aliyetaja likizo kama wakati wa wanafunzi kujumuika na wazazi ili kupata mafunzo kuhusiana na maswala mbalimbali yatakayowasaidia maishani.