Wasiwasi umetanda mtaani Flamingo baada ya mavamizi yaliyotekelezwa eneo hilo na genge linaloshukiwa kuwa kundi la Mungiki. Mashambulizi hayo yalifanywa Jumatano usiku na vijana waliokuwa wamejihami.
“Tayari watu wawili walijeruhiwa vibaya na kuna wasiwasi mkubwa kwani inasemekana kuna kundi linapanga kulipiza kisasi,” alisema Achieng Mmbone.
Tayari polisi wamewatia watu wawili mbaroni kuhusiana na mashambulizi ya siku ya Jumatano na wanazuiliwa katika kituo cha polisi cha Bondeni.
Wakaazi walisema kumekuwa na ripoti kuwa kuna mashambulizi yanayopangwa.
“Polisi wamekosa kuchukulia habari kwa uzito. Kumekuwa na habari hizo baada ya madai ya makaratasi kuangushwa,” mkaazi mwingine alisema.
Wakazi hao waliwataka polisi kuimarisha doria.
Mkuu wa polisi wa utawala Barnabas Kimutai hata hivyo alisema hali ni shwari kwani polisi wamechukua usukani eneo hilo.