Share news tips with us here at Hivisasa

Muungano wa walimu nchini Knut umelaumu baraza kuu la mtihani nchini Knec kwa visa vya wizi wa mtihani ulioshuhudiwa katika mtihani wa kidato cha nne KCSE, wa mwaka jana.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Nairobi muda mchache tu baada ya waziri wa elimu Fred Matiangi kuyatangaza matokeo ya mtihani huo, katibu mkuu wa Knut, Wilson Sossion, amesema ni jambo lisilo haki kuyafutilia mbali matokeo ya wanafunzi ilihali Knec ndiyo yenye jukumu la kuulinda mtihani huo.

“Si haki kumnyima mwanafunzi matokeo yake kwa madai ya wizi. Knec ndiyo inautahini mtihani, kwa hivyo mwanafunzi atakuwa anadhulumiwa kwa makosa yasiyo yake,” alisema Sossion.

Akiyatangaza matokeo ya mtihani wa mwaka jana siku ya Alhamisi, Waziri wa Elimu Dkt Fred Matiang’i alisema kuwa zaidi ya watahiniwa 5,000 walioukalia mtihani huo watakosa matokeo yao baada ya kupatikana na hatia ya kuhusika katika wizi wa mtihani.

Matiangi alisema kuwa visa vya udanganyifu viliongozeka kwa asilimia 70 mwaka uliopita, ikilinganishwa na mwaka wa 2014 ambapo takribani vituo 505 viliripotiwa kuhusika katika wizi huo.

Hata hivyo, Matiang’i alisema kuwa ni matokeo ya mwanafunzi binafsi ambayo yatafutiliwa mbali wala sio ya shule nzima, kama ilivyokuwa katika miaka ya awali.

Aidha, waziri huyo alisema kuwa kaunti 46 nchini zilishiriki udanganyifu wa mtihani isipokuwa kaunti ya Isiolo.