Vijana wawili wenye umri wa miaka 16 na 17 wanauguza majeraha ya panga katika hospitali ya St Elizabeth baada ya genge la vijana kuwashambulia katika mtaa wa Flamingo viungani mwa mji wa Nakuru hapo jana jioni.
Wawili hao Kenneth Mukangare na Geoffrey Mungai walishambuliwa wakielekea nyumbani mwendo wa saa moja usiku.
Wakizungumza katika hospitali hiyo iliyo katika mtaa wa langalanga, wawili hao wamesema kuwa waliona genge la watu waliokuwa wamebeba mapanga na silaha zingine butu ambapo walianza kuwashambulia kabala ya umma kuingilia na kuwasaidia.
Aidha wamesema kuwa genge hilo halikuwaitisha kitu chochote huku wakisema lengo lao kuu likiwa ni kutekeleza mauaji, ambapo walipata majeraha kichwani na mikononi.
Kwa mujibu wa daktari Victor Onsera waliwahudumia vijana na hawako katika hatari.
Kutokana na hilo polisi wakiongozwa na mkuu wa polisi tawala katika mji wa Nakuru Barnabas Kimutai walifika katika eneo hilo na hatimaye kuwakamata washukiwa wawili na kupata panga moja ambalo linadaiwa lilitekeleza mashambulizi hayo.
Washukiwa hao wanazuiliwa katika kituo cha polisi cha bondeni uchunguzi ukiendelea.
Hata hivyo kwa mujibu wa polisi genge hilo lilitokea eneo la Rhonda viungani mwa mji wa Nakuru.
Hata hivyo polisi wameimarisha doria za kiusalama katika mitaa mbalimbali ya mji wa Nakuru.