Serikali ya Ujerumani imetoa jumla ya shilingi milioni 1.4 za kukarabati mfumo wa maji taka katika ziwa la Nakuru.
Kulingana na waziri wa mazingira kwenye kaunti ya Nakuru Richard Rop, kumekuwa na tatizo la ongezeko la uchafuzi katika ziwa hilo akisisitiza kwamba wameweka mikakati ya kukabiliana na utumizi wa plastiki kwenye kaunti ya Nakuru.
Ameongeza kwamba mbuga la wanyama la ziwa Nakuru limeadhiriwa pakubwa na uchafu unaotoka kwenye viwanda pamoja na ule unaosababishwa na ujenzi wa vyumba vya kisasa katika mji wa Nakuru, hatua ambayo sasa ni tishio la uwepo wa ziwa hilo la Nakuru.
Waziri huyo aliyekuwa akizungumza na wanahabari mjini Nakuru hii leo Jumanne tarehe 29 Desemba amehoji kwamba uchafu mwingi kutoka mjini Nakuru na viungani mwake ambao umekuwa ukielekea kwenye ziwa Nakuru umeadhiri maandhari ya ziwa hilo.
Ameongeza kwamba uchafu unaoelekezwa kwenye ziwa hilo kama vile karatasi za plastiki na takataka nyinginezo zinasababisha magugu kuongezeka kwenye ziwa hilo akikariri kwamba uchafuzi huo kwenye ziwa Nakuru umekuwa ukiongezeka kwa muda wa miaka 10 sasa.
Kwa upande wake, afisa mkuu wa ulinzi wa mbuga hiyo ya wanyama pori Dickson Ritan kupitia kwa njia ya simu amesema shirika la wanyama pori la KWS hukusanya hadi kilo 500 za plastiki kila wiki, hatua ambayo anasema ina madhara makubwa kwenye mazingira.