Share news tips with us here at Hivisasa

Maafisa wa polisi huko Kisauni mjini Mombasa wanalisaka genge moja la wahalifu linalodaiwa kuwavamia askari wa kaunti na kuwapiga katika eneo la Bombolulu jana jioni.

Kulingana na naibu afisa mkuu wa polisi katika eneo hilo Walter Abondo, genge hilo lilishirikiana na makondakta wa matatu wanaohudumu katika barabara hiyo waliwapiga askari hao na kuyapiga magari yao kwa mawe hali iliyozua taharuki katika eneo hilo.

Katika purukushani hilo, askari sita walijeruhiwa huku watatu wakigongana na matatu baada ya dereva wa matatu kudaiwa kuwagonga kwa makusudi askari hao.

Askari waliojeruhiwa wanapokea matibabu ya dharura katika hospitali ya kibinafsi ya Sayyida Fatma huko Mlaleo katika eneo hilo la Kisauni.

Mbunge wa eneo la Kisauni Rashid Bedzimba amekashifu tendo hilo na akawataka maafisa wa polisi katika eneo hilo la Kisauni kuwakabili wahalifu hao.