Idara ya Usalama katika eneo la Pwani imependekeza kubuniwe sheria zitakazosaidia kukamatwa kwa watu wanojihusisha na ufisadi.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Ijumaa, Mshirikishi Mkuu wa Utawala eneo la Pwani, Nelson Marwa, alisema kuwa Bunge la taifa linafaa kupitisha sheria kali za kuwakabili wanaoendeleza ufisadi.
Marwa alieleza kuwa visa vya ufisadi vimeongezeka kutokana na mazoea ya wananchi kutoa hongo kwa maafisa wa usalama na idara nyingine za umma ili wahudumiwe kinyume cha sheria.
“Visa vya ufisadi vimeongeza mno katika idara ya usalama na idara zengine za umma na itakuwa vyema iwapo bunge la taifa litapitisha sheria kali za kuwakabili wafisadi nchini ili kupunguza kufujwa kwa mali ya umma,” alisema Marwa.
Kauli yake inajiri huku ripoti ya ufisadi iliyotolewa hivi majuzi ikionyesha kuwa Wizara ya Usalama wa Ndani ndiyo inayoongoza kwa visa vya ufisadi.