Aliyekuwa Kadhi Mkuu wa Kenya Sheikh Hammad Kassim ameishtaki Afisi ya Mkuu wa Sheria Githu Muigai kuhusu uteuzi wa makamishna wa Tume ya Wakf nchini.
Pamoja na viongozi wengine wa dini, Bw Hammad ameishtaki afisi hiyo kwa kile alichokitaja kama kutohusishwa kwa jamii ya Waislamu kabla ya kufanya uteuzi huo.
“Sheria inaipa afisi hiyo jukumu la kuhakikisha wamepata maoni ya jamii ya waislamu kabla ya kuwateua makamishna wa Wakf,” alisema Hammad. “Afisi ya Mkuu wa Sheria haikutushirikisha kupata maoni hayo.”
Hii inafuatia uteuzi wa makamishna wapya Sheikh Juma Ngao, Shariff Hussein Ahmed, Prof Hamadi Boga, Noor Zubeir Hussein, Nagib Shamsan, na Dkt Mwanakitini Bakari.
Wengine wanaoshirikiana na Kadhi huyo wa zamani ni msimamizi wa Msikiti wa Basheikh Bw Naaman Mohamed Naaman, Bw Ali Said Mohamed Al-Mandhry, pamoja na msimamizi wa Msikiti wa Mkanyageni Bw Muhiddin Mohamed Muhiddin.
Wanne hao wamemtaka Jaji Mathew Emukule asimamishe kutekelezwa kwa uteuzi huo hadi korti ifanye uamuzi.