Nchi za kimataifa ambazo zinafadhili miradi mbali mbali ikiwemo shughuli za Tume ya uchaguzi na mipaka IEBC, zimetoa ombi kwa serikali kufanya uchunguzi kuhusiana na vifo vya watu wanne na majeruhi kadhaa wakati wa maandamano ya Cord.
Nchi hizo zimezua tetesi kuwa huenda idara ya usalama ilitumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji hao siku ya Jumatatu.
Wakizungumza na wanahabari jijini Nairobi, mabalozi kumi na wawili kutoka Marekani, Ulaya, Ubelgiji, Norway na Jumuiya ya madola walisema kuna haja ya uchunguzi kufanywa, na kuhimiza mazungumzo yatakayoleta suluhu la kudumu katika swala hilo la IEBC.
Mabalozi hao walisema kuwa ghasia hazitaleta uwiano katika siku za usoni za tume hiyo, wala hazitafanya uchaguzi wa 2017 kuwa wa huru na haki.
"Tunawaomba mkae kwa pamoja mzungumze kuhusiana na swala hili la IEBC. Aidha, tunawaomba kufuata sheria mwafaka iliyowekwa katika kusuluhisha mizozo inayoibuka katika mambo ya kila siku. Tuko tayari kuwaunga mkono wakati wowote mutakapohitaji msaada wetu,” walisema mabalozi hao.