Kamishina wa kaunti ya Kisii Chege Mwangi ameagiza kufungwa kwa viwanda vidogo vidogo vya watu binafsi ambavyo hutengeneza sukari nguru katika eneo bunge la Mugirango Kusini..
Kulingana na Mwangi aliyezungumza mjini Kisii alisema imebainika kuwa sukari nguru ambayo hutengenezwa katika eneo hilo hutumika kupika pombe haramu ambayo ni kinyume na sheria hivyo kumlazimu kuchukua hatua hiyo
“Naagiza vile viwanda vidogovidogo vya watu binafisi vinavyotengeneza sukari nguru Mugirango Kusini kufungwa mara moja,” alisema Mwangi.
“Nimeagiza hilo maana hiyo sukari nguru ndio inatumika kutengeneza pombe haramu na sitakubali kuona pombe hiyo kuendelea katika kaunti yetu ya Kisii maana ulevi haupendezi,” aliongeza Mwangi.
Hatua hiyo imewashangaza wakaazi wa eneo hilo kwani wengi hutegemea biashara ya sukari nguru huku wengine wakisema hawaitumii katika kutengeza pombe pekee ila inatumika kutengeneza vitu tofauti kando na pombe.
“Wengi tunajua hii sukari nguru inatumika kutengeza vitu tofauti wala sio pombe na riziki yetu tunapata kutokana na ukulima wa miwa kwa kutengeneza sukari nguru,” alisema Joseck Kerama mkaazi.