Mwenyekiti wa wadumisha usalama vijijini katika eneo zima la Keroka John Maroko amejitokeza kuwashtumu vikali wanasiasa kwa vurugu zinazoendelea kushuhudiwa kwenye mzozo wa umiliki wa mji huo baina ya serikali ya kaunti ya Nyamira na ile ya Kisii. 

Share news tips with us here at Hivisasa

Akihutubia wanahabari siku ya Alhamisi, Maroko alisema kuwa vurugu zinazoendelea kushuhudiwa katika eneo hilo zinatokana na uchochezi unaosababishwa na baadhi ya wanasiasa. 

"Ukweli ni kuwa vurugu zinazoendelea kushuhudiwa katika eneo hili hazitokani kwa sababu ya mzozo wa kimpaka kati ya serikali ya kaunti ya Nyamira na ile ya Kisii, ila ni kutokana na jumbe za uchochezi ambazo baadhi ya wanasiasa wanaendelea kuzisambaza miongoni mwa wananchi," alisema Maroko. 

Maroko aidha alisema kuwa kufuatia vurugu hizo zinazoendelea kushuhudiwa katika eneo hilo, wadumishaji usalama wamepata ugumu wa kulinda watu wasipigane, hali aliyosema yafaa mkurugenzi wa mashtaka Keriako Tobiko aingilie kati ili kuchunguza wahusika na kuwachukulia hatua kali. 

"Vita ambavyo tunaendelea kuvishuhudia hapa vinatokana na uchochezi wa watu fulani wachache na ndio sababu twamtaka Keriako Tobiko kuingilia kati na kuchunguza suala hili ili wahusika wachukuliwe hatua za kisheria kwa maana sisi wadumishaji usalama tumekuwa na changamoto za kulinda watu wasipigane kwasababu ya mzozo huu," aliongezea Maroko.