Serikali ya Ufaransa imeahidi kushirikiana na serikali ya kaunti ya Mombasa katika jitihada za kuimarisha sekta ya utalii nchini.
Afisa mkuu wa maswala ya utamaduni nchini Ufaransa Jean-Pierre Tutin amesema kwamba serikali ya ufaransa imeondoa marufuku ya raia wao kuzuru Mombasa na Malindi kufuatia misukosuko ya kiusalama iliyoshuhudiwa hapo awali.
Akiongea mjini Mombasa siku ya Alhamisi katika kikao cha wadau wa utalii, Tutin alisema kwamba sekta ya utalii itaimarika kwa kiwango kikubwa kufuatia idara ya usalama nchini kuimarisha usalama katika eneo la Pwani.
Aliongezea kwa kusema kwamba serikali ya Ufaransa iko tayari kuisaidia Kaunti ya Mombasa.
"Tuko tayari kusaidiana na Kaunti ya Mombasa kuimarisha sekta ya utalii na utamaduni. Serikali yetu imeondoa marufuku tuliyokuwa tumeweka kwa raia wetu kuzuru Mombasa na Malindi. Sasa watakuja na kujivinjari kwa sababu tumeona eneo la Pwani liko salama,” alisema Tutin.
Mkuu wa idara ya utalii katika Kaunti ya Mombasa Binti Omar alipongeza juhudi hizo na kusema kwamba kuondolewa kwa marufuku hiyo na taifa la Ufaransa kutainua uchumi wa taifa hili hasa ikizingatiwa kuwa utalii ndio kitega uchumi wa eneo la Pwani.
Binti alisema kuwa hatua hiyo huenda ikaboresha zaidi tamaduni za eneo hili na kuwavutia wageni na watalii wengi zaidi kuzuru eneo la Pwani na hususan Kaunti ya Mombasa.
"Tumeshukuru sana taifa la Ufaransa kuondoa marufuko hiyo na sasa tunatarajia wageni wengi kutoka Ufaransa kuzuru Mombasa na Malindi. Hatua hii itaimarisha zaidi sekta ya utalii na kukuza uchumi wetu,” alisema Binti.
Hatua ya taifa la Ufaransa kuondoa marufuku hiyo imejiri miezi michache tu baada ya taifa la Uingereza na Marekani kuondoa maruku ya raia wao kuzuru humu nchini na hususan eneo la Pwani, kama njia mojawapo ya kuimrisha sekta ya utalii.