Share news tips with us here at Hivisasa

Shirika lisilo la serikali la Joy Foundation limeanzisha mikakati yakuhakikisha kuwa wakazi wa Nyamira wanapata maji safi ya kunywa.

Kulingana na mkurugenzi wa shirika hilo, Joy Kerubo, shirika hilo litahakikisha kuwa wakazi wa Gusii wanapata maji safi ya kunywa, kwa kuwa maji ni muhimu sana kwa afya ya wananchi.

"Maji ni muhimu sana katika maisha ya wananchi na sisi kama shirika tumeweka mipango yakuhakikisha kuwa wakazi wa maeneo ya Gusii wanapata maji safi ya kunywa na pia ya matumizi yao ya nyumbani," alisema Kerubo.

Afisa mshirikishi wa shirika hilo Kefa Osiri alisema kuwa mradi huo ambao tayari umeanzishwa katika eneo bunge la Kitutu Masaba utasambazwa kwenda kwa maeneo mengine kabla ya mwaka ujao kutamatika ili kuwanufaisha wakazi wengi.

"Tumeanzisha mikakati yakuhakikisha kuwa wakazi wa eneo la Nyamira wanapata maji safi kwa matumizi yao na tayari tushaanza kukarabati visiwa na chemechemi za maji ili kuhakikisha kuwa maji hayaathiriwi vyovyote na kusababishia wakazi magonjwa. Nina furaha kueleza kuwa mradi huu utahakikisha kuwa shule na soko zimepata maji kwa njia ya mifereji," alisema Osiri.

Osiri aliwahimiza wakazi wa kaunti hiyo kuchangamkia hatua hiyo ya usambazaji maji kukumbatia kilimo ili kuimarisha maisha yao, huku akisisitiza kuwa mradi huo ni wakuwasaidia wananchi wala sio wa kisiasa.

"Sote tunafahamu kuwa ili kilimo kustawi, sharti kuwepo na maji na ndio maana nawahimiza wakazi wa maeneo yatakayo faidi kutokana na mradi huu kuchukua hatua ya kujihusisha na kilimo. Iwapo watazingatia hili pasina shaka watanufaika pakubwa kiuchumi,”alisema Osiri.