Mkurugenzi wa wizara ya elimu katika kaunti ya Nyamira Siloma Kinaiyo amekanusha madai ya wakazi wa kaunti hiyo kwamba walimu wa shule ya msingi ya Nyakemincha walihamishwa kwasababu za kisiasa.
Akihutubia wanahabari ofisini mwake siku ya Jumatano, Kinaiyo alisema tume ya uajiri wa walimu TSC ililazimika kuchukua hatua hiyo ili kuimarisha matokeo ya shule hiyo ambayo kwa muda imekuwa ikifanya vibaya kwenye mitihani ya kitaifa KCPE.
"Tume ya uajiri wa walimu nchini ndiyo iliyoamua kuwahamisha walimu wote wa shule ya msingi ya Nyakemincha baada ya ripoti ya jopo la kamati iliyoteuliwa kuchunguza suala hilo kupendekeza hatua hiyo ili kuhakikisha kuwa viwango vya elimu vinaimarika," alisema Kinaiyo.
Afisa huyo aidha aliwaonya vikali walimu waliohamishiwa shule hiyo kutokana na kutoripoti kwao shuleni kwa wakati unaofaa huku akisema kwamba watachukuliwa hatua kali zakinidhamu.
"Kuna ripoti zinazonikifia ofisini mwangu kwamba baadhi ya walimu waliohamishiwa shule ya Nyakemincha wangali kuripoti shuleni ila ni onyo kwao kwa maana serikali haitasita kuwachukulia hatua za kinidhamu baada ya muda waliopewa kuhama kukamilika," Kinaiyo alisema.