Shughuli za uchukuzi katika barabara kuu ya kutoka Mombasa kuelekea Jijini Nairobi zimekatizwa baada ya barabara hiyo kufungwa ili kutoa nafasi kwa shughuli za ujenzi zinazoendelea katika barabara hiyo.
Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari iliyotiwa saini na Halmashauri ya barabara kuu nchini, barabara hiyo imefungwa ili kutoa nafasi kwa ujenzi wa madaraja na barabara nyingineyo inayounganisha ile ya reli katika eneo la Taru.
Kulingana na taarifa hiyo barabara hiyo itafungwa kwa siku nzima siku ya Jumatato na itafunguliwa saa kumi na mbili jioni kuruhusu shuhuli za usafiri.
Kwa sasa Madereva wanalazimika kutumia barabara mpya ya reli ili kupita eneo hilo , hali ambayo Madereva wengi wamelalamikia kuwa imewalazimisha kucheleweshwa safari zao hasa wale madereva wa magari ya masafa marefu.
"Imetulazimu kuchukua muda mrefu kusafari kwa sababu ya ujenzi wa daraja lakini tuko na imani shuhuli yenyewe haitachukua siku nyingi kama walivyosema wahusika wakuu",alisema mmoja wa madereva wa masafa marefu Micheal Nderitu siku ya Jumatano.
Kwa muda wa takriban miaka miwili sasa, Madereva wanaotumia barabara hiyo ya kutoka Mombasa kuelekea Nairobi wamekuwa wakilalamikia misongamano ya mara kwa mara.