Mamia ya waumini wa Kanisa Katoliki mjini Mombasa wameungana na wenzao ulimwenguni kuadhimisha mwanzo wa sikukuu ya Pasaka inayotanguliwa na siku ya Ijumaa Kuu.

Share news tips with us here at Hivisasa

Misafara mirefu ilionekana katika barabara za mji wa Mombasa huku waumini wakibeba misalaba wakiwa wanaomba pamoja na kuimba nyimbo za kukumbuka mateso ambayo Yesu Kristu aliyapitia.

Akiwahutubia waumini wa Kanisa Katoliki la Holy Ghost Cathedral mjini Mombasa, Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Mombasa Askofu Martin Kivuva, aliwasihi Wakirstu kuzingatia mafundisho ya dini wakati wanaposheherekea Pasaka.

“Wakristu munafaa kukumbaka mateso ambayo Yesu Kristu aliyapitia na kuwa wanyenyekevu na kuzingatia mafunzo ya dini ili kuwa waumini wa kumpenda Mungu na kuwasaidia wasiojiweza,” alisema Askofu Kivuva.

Askofu Kivuva alisema kwamba taifa la Kenya linakaribia kipindi cha uchaguzi mkuu wa mwaka 2017, na linahitaji maombi.

Aidha, kiongozi huyo wa dini aliwahimiza Wakristu washirikiane katika kupiga vita ufisadi nchini.

“Taifa hili inakaribia kipindi cha uchaguzi mkuu. Tafadhali tuliweka taifa letu katika maombi na kuwa katika mstari wa mbele kupiga vita ufisadi, ndio tuweze kuwa na maendeleo nchini,” aliongeza Askofu Kivuva.

Wakristu wanatarajiwa kushiriki ibada maalum ya kuadhimisha mkesha wa kufufuka kwake Yesu Kristu usiku wa siku ya Jumamosi.