Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Watoto wanaoranda randa mitaani jijini Kisumu, wametoa wito kwa serikali kuu, serikali ya kaunti na wadau wengine yakiwemo mashirika ya kijamii, kuwasaidia kuimarisha hali yao ya maisha.

Wakizungimza na mwandishi huyu kwenye mahojiano, baadhi ya watoto hao walielezea changamoto wanazokabiliana nazo katika maisha yao ya kila siku.

Watoto hao walisema kuwa wanakabiliwa na ukosefu wa chakula, mahala pa kuishi na kulala, na magonjwa, hasa msimu huu wa mvua inayozidi kunyesha katika maeneo mbali mbali nchini.

Wakiongozwa na Vincent Kipchumba, watoto hao walisema kuwa pesa wanazoomba kutoka kwa wapita njia ndizo zimekuwa zikimudu mahitaji yao, ila baadhi ya wapita njia hao huishia kuwapiga na hata kuwafukuza.

“Tunalala nje na kila wakati tunakua wagonjwa kutokana na kupigwa na baridi. Kupata chakula ni shida na inabidi tuombe wapita njia. Wakati mwingine ukiomba mtu anakunyima au anakupiga,” alisema Kipchumba.

Aliongeza, “Tunaomba usaidizi kutoka kwa wahisani waweze kutujengea mahali pa kuishi na pia kutupa nafasi ya kusoma. Itakuwa vyema iwapo tuatapata elimu, ili nasi pia tuweze kuwasaidia wengine.”

Kipchumba alitoa wito kwa wahisani, kujitokeza kuwasaidia watoto wanao randaranda mitaani, akisema kuwa wao ni watoto kama wengine na sio kupenda kwao kurandaranda mitaani.