Maafisa wa polisi mjini Mombasa wamewatia nguvuni washukiwa watatu wa ugaidi wanaoaminika kupanga njama ya kutekeleza mashambulizi ya kigaidi mjini humo.
Kulingana na maafisa hao, washukiwa hao watatu walikamatwa katika chumba kimoja cha kukodi katika hoteli moja eneo la Bondini mjini Mombasa wakiwa na vitambulisho bandia, simu za rununu tatu, bunduki aina ya AK47 na risasi 54.
Akithibitisha kutiwa nguvuni kwa washukiwa hao wa ugaidi mjini Mombasa siku ya Jumatano, Afisa mkuu wa polisi Kisiwani Mombasa Martin Asin amesema kwamba washukiwa hao wataendelea kuzuiliwa na maafisa wa polisi pamoja na kufanyiwa mahojiana na maafisa wa kitengo cha kupambana na ugaidi kabla ya kufikishwa mahakamani.
"Maafisa wetu wa polisi wamewakamata washukiwa watatu wa ugaidi katika chumba cha kukodi kwenye hoteli moja eneo la Bondeni na wanazuiliwa kwa sasa na kufanyiwa mahojiano kabla ya kufikishwa mahakamani. Maafisa wa polisi wako macho kuhakikisha usalama unaimarisha na kuzuia mashambulizi ya kigaidi", alisema Asin.
Aidha Asin amewatahadharisha wakaazi wa kaunti ya Mombasa dhidi ya washukiwa wa ugaidi na akawataka kuwa katika mstari wa mbele kutoa habari muhimu kuhusu washukiwa wa ugaidi ili maafisa wa polisi wawatie nguvuni na kuzuia mashambulizi.
Tukio hilo limejiri baada ya maafisa wa polisi kuimarisha doria katika kaunti nzima ya Mombasa tangu shamra shamra za sherehe za krismas na mwaka mpya kuanza kote nchini.
Vifaa ya kutekelezwa mahsambulizi mjini Mombasa vikakaguliwa na maafisa wa polisi baada ya washukiwa watatu wa ugaidi kutiwa nguvuni na maafisa wa polisi.