Serikali ya Kaunti ya Nyamira imehimizwa kupandisha hadhi ya Hospitali ya Riomego iliyoko katika eneo bunge la Mugirango Kaskazini hadi level Four, ili kutoa huduma bora za matibabu.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akizungumza siku ya Jumapili katika eneo la Mawawa, Naibu Gavana wa Kaunti ya Nyamira Amos Nyaribo, aliiomba serikali ya Kaunti ya Nyamira kupitia Gavana John Nyagarama, kupandisha hadhi ya hospitali hiyo kwa kusema kuwa huduma ambazo zinatolewa kwa sasa sio za kuridhisha.

“Huduma za matibabu zinazotolewa katika Hospitali ya Riomego sio kamilifu kutokana na ukosefu wa madaktari na dawa za kutosha. Ninaomba Gavana Nyagarama kuboresha hospitali hii hadi kiwango cha Level Four ili kuimarisha sekta ya afya zaidi,” alisema Nyaribo.

Aidha, Nyaribo aliiomba kaunti hiyo kuchimbia wakaazi wa eneo la Mawawa visima vya maji kwa kuwa akina mama hulazimika kutembea kwa muda mrefu ili kupata maji.

“Naomba serikali kuwapa afueni akina mama kutokana na ukosefu wa maji kwa kuchimba visima hapa Mawawa,” aliongeza Nyaribo.