Mwakilishi wa wadi ya Manga James Maroro amejitokeza kuwashtumu baadhi ya wawakilishi wadi kwenye bunge la kaunti ya Nyamira kwa kudinda kuidhinisha ripoti ya kamati ya uwekezaji na uhasibu wa pesa za umma.
Akiwahutubia wanahabari mda mchache baada ya kikao cha kujadili ripoti hiyo kutamatika siku ya Jumatano, Maroro alisema kuwa ni aibu kubwa kwa bunge hilo kukataa kuidhinisha ripoti ambayo ilikuwa ya umuhimu kukabili maafisa wafisadi serikalini.
"Ni aibu kubwa kwa bunge hili kukataa kuidhinisha ripoti ambayo ingewalazimu baadhi ya maafisa wakuu serikalini kurejesha pesa zilizovujwa kwa kisingizio cha kufadhili miradi,” alisema Maroro.
Maroro aidha aliongeza kwa kuwaonya wawakilishi wadi dhidi ya uamuzi huo, suala alilohoji kwamba huenda likatumiwa na wapiga kura kuwaondoa mamlakani baadhi ya wawakilishi wadi.
“Huenda historia ikawahukumu vibaya wale wawakilishi wadi waliopinga ripoti ya PIAC kwa maana wananchi huenda wakatumia kukataliwa kwa ripoti hii kuwaondoa afisini wale waliopinga ripoti hii,” aliongezea Maroro.