Serikali ya Kenya kupitia kwa Wizara ya usalama wa ndani imeandaa mazungumzo na mataifa mengine kama vile Rwanda, Uganda na Sudan Kusini kubuni sheria za kuwawezesha wafungwa waliohukumiwa nchi za nje kutumikia vifungo vyao katika nchi zao.

Share news tips with us here at Hivisasa

Kwa mujibu wa katibu wa kudumu katika wizara hiyo Micah Powon, sheria hizo zinanuia kuwawezesha wafungwa kuwa karibu na familia zao na pia kurekebisha tabia kwa njia inayofaa kulingana na sheria za nchi zao.

Powon pia amedokeza kuwa kuna zaidi ya wafungwa 800 kutoka Kenya ambao wamefungwa katika nchi za kigeni.

“Nchi hizo zinatumia lugha za kigeni na hivyo basi ni vigumu kwa wafungwa hao kurekebishwa kwa lugha ambayo hawaielewi,” alisema Powon.

Takwimu za hivi majuzi zinaonyesha kuwa wengi wa Wakenya walioshtakiwa na kufungwa jela katika nchi za kigeni ni wale ambao wamepatikana na kosa la ulanguzi wa mihadarati.

Powon alisema haya baada ya kukutana na wajumbe wa wizara ya gereza kutoka Uganda,Rwanda na Sudan Kusini siku ya jumatano mjini Mombasa.