Zaidi ya waendeshaji bodaboda 100 kutoka kaunti ya Nakuru walifanya maandamano siku ya Alhamisi kulalamikia kuhangaishwa na kunyanyaswa na maafisa wa polisi.
Maandamano hayo yalianza baada ya mmoja wa wahudumu hao wa bodaboda kujeruhiwa alipodinda kukamatwa na afisa wa polisi karibu na kituo cha kibiashara cha Free area kilicho viungani mwa mji wa Nakuru.
Wahudumu hao walisema kuwa mwenzao aligonga kalvati na kuingia mtaroni baada ya afisa mmoja wa polisi kuzuia pikipiki yake alipokuwa akijaribu kutoroka.
Mhudumu huyo alipelekwa katika hospitali ya mkoa wa bonde la ufa iliyo mjini Nakuru ambapo anauguza majeraha kwa sasa.
Mmoja wa waendeshaji bodaboda aliyehojiwa na wanahabri kwa jina la Isaac Mukundi alisema maafisa wa polisi, hasaa walio katika eneo la Hyrax wamefanya maisha yao kuwa magumu baada ya kuwanyanyasa licha ya kuwa wametimiza masharti yote wanatoyakiwa.
Aidha, wahudumu hao walitaka kujua ni kwa nini wanalaumiwa kwa visa vya ukosefu wa usalama katika eneo hilo, wakisema hatua hiyo imewapelekea kuziwa kuingia mitaani na mabawabu wa mitaa hiyo.
Mwakilishi wa wadi ya Menengai Michael Macharia alikashifu tendo hilo la unyanyasaji wa wahudumu wa bodaboda akihoji kuwa wameripoti tukio hilo kwa OCPD wa Nakuru Musa Kongoli, ambaye anaendeleza uchunguzi kwa sasa.
Hata hivyo, aliwahimiza waendeshaji bodaboda hao kuhakikisha wanazingatia masharti yote wanayotakiwa ili kuwawezesha kuendeleza biashara yao, hatua aliyosema itazuia mgongano kati yao na maafisa wa polisi.