Mkuu wa polisi katika Kaunti ya Kisii Simon Kiragu amewaomba wakazi wa kaunti hiyo kuripoti mzazi yeyote anayemnyima mtoto wake haki ya masomo ili kuchukuliwa hatua kali ya kisheria.
Wito huo umetolewa baada ya kanisa moja mjini Kisii kwa jina Mount Love Church kukataza waumini wake kutowapeleka watoto wao shuleni kufundishwa, kutoajiriwa kufanya kazi na kutopeleka mtu hospitali anapougua.
Jambo hilo limezua mjadala katika kaunti hiyo, huku mwanamke mmoja akilazimika kuvunja ndoa yake na kutoroka baada ya kuwanyima watoto wake haki ya masomo.
Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumanne mjini Kisii, Kiragu aliwaonya wazazi wanaowanyima wanao haki ya masomo, na kusema watakapofumaniwa watachukuliwa hatua kali ya kisheria.
Aidha aliwaomba wakazi kupiga ripoti kwa kituo chochote cha polisi ikiwa watashuhudia mzazi anayefanya kitendo kama hicho ili kuchukuliwa hatua za kisheria.
“Naomba wakazi wa kaunti hii kuripoti kisa chochote watakishuhudia kwa wazazi wanaowanyima watoto wao haki ya masomo, kwa sababu hiyo ni kinyume na sheria,” alisema Kiragu.
Aidha, afisa huyo aliomba wazazi kuwapeleka wanao shuleni na kutowadhulumu kimasomo kwani masomo ndio msingi wa maisha.