Wakaazi wa Kaunti ya Nakuru sasa wanaweza kubaini famasi zilizoidhinishwa na kuruhusiwa kuuza dawa kupitia kwa mchoro wa msalaba wa rangi ya kijani ambao uko kwenye upande wa mbele wa famasi hizo.
Akizungumza kwenye mahojiano na mwandishi huyu mjini Nakuru siku ya Alhamisi, mfamasi mkuu Kaunti ya Nakuru Dkt Simon Wangia alitaja mbinu hiyo kama njia moja ya kuwasaidia wakaazi wa Nakuru kujiepusha na ununuzi wa dawa gushi.
“Tuna muungano unaofahamika kama wa kijani kibichi kati ya wanafamasia. Famasi zinazoendelezwa na wanafamasia walioofuzu zimechorwa msalaba wa kijani kibichi nje. Hatua hiyo inabaini kuwa famasi hizo zimesajiliwa,” alisema Wangia.
Alisisitiza kuwa wanajibidiisha kuhakikisha wakaazi wa Nakuru hawanunui dawa gushi ambazo huenda zikawaletea madhara, kupitia hafla mbalimbali kama hamasisho kuhusiana na wanafamasia.
“Tuna wiki ya kuwahamasisha wakaazi inayojulikana kama 'Pharmacy Awareness week'. Mwaka jana tulikuwa na hafla ambazo tulikuwa tunatumia kuhamasisha wakaazi kupitia kwa vijikaratasi pamoja na habari kuhusiana na muungano huo wa msalaba wa kijani,” aliongeza Wangia.
Wakati huo huo, aliwashauri wale wanaoathiriwa na dawa wanazonunua kutoka kwa famasia kufika katika hospitali za umma ambapo wafanyikazi wa afya katika hospitali hizo, watachukua maelezo na kisha kuyatuma katika bodi ya dawa na sumu.
Alisema kuwa hatua hiyo itawawezesha wanafamasia gushi kukamatwa.