Mwenyekiti mpya wa wafanyabiashara wa kaunti ya Nyamira Joseph Misati ameahidi kufanikisha pakubwa uimarishaji wa mazingingira ya kibiashara katika eneo hilo.

Share news tips with us here at Hivisasa

Misati, ambaye alichaguliwa kuwaongoza wafanyabiashara hao kwa mda wa miaka mitatu, aliwahutubia wanahabari baada ya kuchaguliwa kwake siku ya Alhamisi na kuahidi kuwa kabla ya mwaka wa kwanza kukamilika atahakikisha kuwa muungano wa wafanyabiashara umepata kipande cha ardhi patakapojengwa ofisi zao. 

"Kwanza ningependa kuwashukuru wafanyabiashara waliojitokeza kunipigia kura leo hii, na kwa kweli lile nitakalohakikisha kuwa nimelitekeleza ni kuhakikisha kuwa kama muungano tumepata kipande cha ardhi tutakapojenga ofisi zetu," alisema Misati. 

Kutokana na hali ya wafanyabiashara wa soko mbalimbali katika kaunti hiyo kuendelea kuzushia kutolipa kodi kwa sababu ya kulalamikia huduma duni kutoka kwa serikali ya kaunti hiyo, Misati aliahidi kuhakikisha kuwa wafanyabiashara hao wameanza kulipa kodi. 

"Nina ufahamu kuwa baadhi ya wafanyabiashara hasa kwenye soko la Miruka na Keroka wamekuwa wakizushia ulipaji kodi kwa kile wanacholalamikia kuwa ukosefu wa huduma bora kutoka kwa serikali ya kaunti, ila vile ambapo nimechaguliwa hii leo sharti nihakikishe kuwa serikali inawapa huduma bora ili nao walipe kodi kwa kuwa bila kodi hamna maendeleo," aliongezea Misati.