Kamanda wa polisi wa Mombasa Francis Wanjohi amesema kuwa wanaondesha biashara za ulanguzi wa mihadarati katika eneo la Pwani watakabiliwa kwa mujibu wa sheria.
Akizungumza baada ya kukamatwa kwa washukiwa wawili wa ulanguzi wa mihadarati huko Mtwapa, Wanjohi alisema kuwa serikali ipo imara katika vita dhidi ya dawa za kulevya.
Alisema kuwa hawatalegeza kamba katika vita hivyo kwa kuwa vijana wengi katika ukanda wa Pwani wanaendelea kuathirika kufuatia utumizi wa dawa hizo.
Washukiwa hao walikamatwa baada ya mipango yao kutibuliwa na maafisa wa polisi kwa ushirikiano na wakaazi.
Polisi walisema kuwa jamaa hao ni miongoni mwa wahalifu wanaosakwa na maafisa wa usalama eneo la Pwani, kutokana na kuhusika katika biashara hiyo ya dawa za kulevya.
Maafisa hao walisema kuwa bhangi hiyo ilikuwa yenye thamani ya takriban elfu mia tano.
Eneo la Pwani limekuwa likikumbwa na changamoto ya ulanguzi wa mihadarati huku kisa cha hivi majuzi kikishuhudiwa Mariakani, Kaunti ya Kilifi, ambako misokoto mingine ya bhangi ilipatikana.
Mshirikishi wa kanda ya Pwani Nelson Marwa ameagiza maafisa wa usalama kuwa waangalifu na wakaazi wanaojihusisha na biashara hiyo.
Marwa alisema kuwa huenda wanaoedesha biashara hizo wakawa wanapata msukumo kutoka kwa baadhi wa viongozi wa siasa.