Mbunge wa Mswamweni Suleiman Dori amekanusha madai kwamba alimtimua Gavana wa Kwale Salim Mvurya kutoka chama cha ODM.
Dori ambaye hivi majuzi aliunga mkono kauli ya kuwataka viongozi walioasi chama cha ODM kujiuzulu, alisema kuwa hajawahi kutoa matamshi yoyote ya kumtaka Mvurya kugura chama hicho.
Akizungumza katika eneo bunge la Ganze, Dori alisema kuwa madai ya Mvurya kutimuliwa kutoka ODM ni uvumi tu usiokuwa na ukweli wowote, huku akimtaja gavana huyo kama msaliti mkuu wa wakaazi wa Kwale.
“Kutoelewana kupo katika maswala ya kisiasa. Kutofautiana baina yetu ni kwa msingi wa kisiasa wala sio kibinafsi kama inavyochukuliwa na baadhi ya viongozi wenzangu hapa Pwani walioamua kujitenga na mrengo wa Cord,” alisema Dori.
Haya yanajiri baada ya Gavana Mvurya kusema kuwa alichukua uamuzi wa kujitenga na chama cha ODM kutokana na mpango fiche wa kumnyima tiketi ya kuwania wadhifa wa ugavana mwaka ujao.
Alisema kuwa aliposikia tetesi za kunyimwa tiketi, aliamua kuchukua uamuzi huo pasi kuwahusisha wadau wengine katika mrengo wa Cord.
Alidai kuwa anafahamu njama zote zilipangwa na Dori, kutokana na uhasama ambao wamekuwa nao tangu kuingia madarakani kwenye serikali za ugatuzi.
Dori aidha amewahakikishia wakaazi wa Pwani kuwa chama cha ODM ndicho kitakacho angazia maslahi yao, na kuwataka kutupilia mbali sera za viongozi waasi kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.