Wafanyakazi wanane kutoka Halmashauri ya bandari nchini KPA na Halmashauri ya ukusanyaji ushuru nchini KRA, wameachiliwa kwa dhamana ya shilingi laki tano kwa madai ya kuhusika katika kupotea kwa makasha 121 katika bandari ya Mombasa.
Mohamed Ibrahim Hassan, na wengine saba wanadaiwa kuhusika katika kupotea kwa makasha hayo yenye thamani ya shilingi milioni 82, kati ya Mei 1, hadi Agosti 3, mwaka huu.
Wote walikanusha mashtaka hayo katika Mahakama ya Mombasa siku ya Jumanne.
Mahakama pia imetoa agizo la kukamatwa kwa wafanyikazi wengine wanne wanaokabiliwa na madai sawia na hayo.
Hii ni baada ya washukiwa hao kukosa kufika mahakamani.
Kesi hiyo itatajwa Novemba 15 mwaka huu.