Serikali ya kaunti ya Nakuru imetoa hakikisho kwamba itazidi kuzisaidia familia zilizokimbilia kaunti hiyo kutokana na machafuko yaliyotokea kwenye eneo la Olposimoru kaunti ya Narok.
Hakikisho hilo lilitolewa na naibu wa gavana wa kaunti ya Nakuru Joseph Ruto, kwa familia mia sita themanini ambazo zimekita kambi katika shule ya upili ya Olenguruone DEB.
Akizungumza alipotoa msaada wa vyakula, dawa na blanketi kwa wahasiriwa hao, Ruto aliashiria kuwa serikali ya Nakuru itaungana na familia hizo zilizolazimika kuhama makwao wanapopitia wakati huo mgumu.
Aidha, aliongeza kuwa kaunti ya Nakuru inafanya kazi kwa pamoja na shirika la msalaba mwekundu na wadau wengine kuhakikisha kuwa familia hizo zinapokea usaidizi.
Aliweka bayana kuwa serikali yake itazidi kuzisaidia familia hizo hadi pale zitakaporejea makwao, huku akiongeza kuwa serikali za kaunti na ile ya kitaifa zimejitolea kuhakikisha kuwa amani inarejeshwa kwenye eneo hilo.
Kwa mujibi wake, watu wote ambao wameadhirika na mzozo huo watasaidiwa katika muda wa wiki moja kurejea makwao.
Wakati huo huo, Ruto amekanusha madai kuwa mzozo kwenye eneo hilo unahusisha jamii mbili pekee kutoka kaunti za Nakuru na Narok .
Kando na hayo, amewaonya vijana dhidi ya kutumiwa kuzua ghasia.