Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mkurugenzi wa mashtaka ya umma Keriako Tobiko ameunga mkono kuondolewa kwa hukumu ya kifo huku akisisitiza kuwa kifungo hicho ni kinyume cha sheria.

Tobiko anasema sheria zilizopo zinafaa kufanyiwa marekebisho ili kutoa fursa kwa jaji au hakimu kutumia mamlaka yake kutoa adhabu hii kwa waliopatikana na hatia kwa kuzingatia ushahidi uliopo.

Kwa mujibu wa Tobiko, ruhusa ya hukumu itakayopitishwa iwe katika mamlaka na uwezo wa aidha jaji ama hakimu aliyeisikiza kesi na ambao hawakuwa wanaelekezwa na sheria inayoamuru adhabu ya kifo iwe ya lazima.

"Tukizingatia kifungu cha 204 cha katiba, hukumu ya kifo ni kinyume cha sheria. Tuwache bunge iwajibikie majukumu yake na mahakama ifanye kazi yake," alisema Tobiko kupitia kwa wakili wake Njagi Nderitu.

Kuna zaidi ya watu 2,511 katika nchi ya Kenya waliohukumiwa kifo huku wengine 4,203 wakihukumiwa kifungo cha maisha.

Majaji wa mahakama ya juu Willy Mutunga, Kalpana Rawal, Jackton Ojwang, Mohammed Ibrahim, Njoki Ndungu na Smokin Wanjala watatoa taarifa ya uamuzi wa iwapo majaji na mahakimu wametwikwa jukumu la kuamua iwapo hukumu hiyo ya kifo inafaa kuondolewa au la.