Jamii ya Wanubi nchini imeitaka serikali kuu kuwaeleza bayana iwapo inawatambua kuwa kati ya makabila ya Kenya.
Akiongea na wanahabari siku ya Ijumaa mjini Mombasa wakati wa sherehe za tamaduni ya jamii hiyo, katika uwanja wa Mama Ngina, Mwenyekiti wa masuala ya utamaduni na michezo katika jamii hiyo Ibrahim Ambar, alilalama kuwa serikali haijawaorodhesha Wanubi katika makabila ya humu nchini.
Ambar ameitaka serikali kuiorodhesha jamii hiyo kuwa kati ya makabila ya Kenya huku akisema kuwa hatua ya serikali kukosa kuwajumuisha katika maswala muhimu nchini inaonyesha wazi kuwa haiwatambui.
“Tunakata serikali kuwa wazi na kueleza iwapo Jamii ya Wanubi inatambulika kati ya makabila mengini nchini kwa sababu sisi pia ni wakenya,” alisema Ambar.
Aidha, Ambar alilalamikia hatua ya serikali kutoikabidhi jamii hiyo ardhi.