Wizara ya Elimu nchini imehimizwa kuweka mazingira bora kwa wanafunzi ili kufanikisha matokeo bora ya mitihani ya kitaifa.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mwenyekiti wa muungano wa walimu wakuu nchini Dorothy Kamwilu amesema kuwa iwapo serikali itatenga fedha za kutosha kugharamia mahitaji ya shule, basi changamoto zilizopo kwa sasa zitakabiliwa.

Akizungumza katika kongamano la walimu wakuu nchini katika hoteli moja mjini Mombasa siku ya Jumatano, Kamwilu alisema kuwa walimu wakuu wanapitia changamoto nyingi na lazima serikali kuingilia kati.

"Kuna umuhimu wa serikali kuweka mazingira bora ya wanafunzi shuleni ili kuwawezesha kufanya vyema kwa mitihani yao. Shule nyingi ziko katika hali duni na hazina hata vifaa vya kusomea,” alisema Kamwilu.

Akigusia swala la wizi wa mitihani, Kamwilu alisema kuwa tayari walimu wakuu wamepanga mikakati ya kukabiliana na swala hilo ili kuzuia wanafunzi kushiriki udanganyifu wa mitihani.

Aidha, amewataka walimu wakuu kuhakikisha kuwa wanawafunza wanafunzi maswala ya maadili mema kama njia mojawapo ya kuwawezesha kujiepusha na migomo ya mara kwa mara.

Kongamano hilo lilihudhuriwa na zaidi ya walimu wakuu 105 kutoka maeneo mbalimbali nchini kujadili maswala muhimu yatakayoimarisha viwango vya elimu shuleni.