Serikali ya kaunti ya Kisii imeombwa kubadilisha usimamizi kwa wauguzi katika kaunti hiyo ili kuimarisha sekta ya afya kikamilifu.
Wito huo umetolewa baada ya kubainika kuwa idadi nyingi ya kutoa matibabu katika hospitali za Kisii hutolewa na wauguzi hadi kiwango cha asilimia 87.
Akizungumza siku ya Jumanne katika chumba cha mikutano katika hospitali ya rufaa na mafunzo iliyoko mjini Kisii, mwenyekiti wa wauguzi katika kaunti ya Kisii Joseph Keriama aliomba serikali ya kaunti hiyo kuunda kiti cha ukurugenzi kwa wauguzi katika kaunti hiyo kwani wauguzi ndio wengi ikilinganishwa na wengine katika sekta ya afya na kusema kuna haja ya wauguzi kuwa na mkurugenzi wao kando na yule wa afya kwa ujumla.
Kulingana naye kiti hicho kinastahili kuundwa ili kutoa huduma bora pamoja na usimamizi kwa wauguzi huku akisema wauguzi ndio husaidia pakubwa kwa kutoa matibabu katika kaunti hiyo.
Pia aliomba kiti cha unaibu wa ukurugenzi kwa wauguzi kuundwa na kusema ikiwa serikali haitakubaliana na maombi yao watatoa mwelekeo wao kamili baadaye.
“Tunaomba serikali ya kaunti ya Kisii kuunda nafasi ya kiti cha ukurugenzi kwa wauguzi katika kaunti ya Kisii pamoja na unaibu wa kiti hicho ili kuimarisha sekta ya afya kikamilifu,” alisema Joseph Keriama.
“Katika sekta hii ya afya wauguzi ndio wengi kwa kutoa matibabu na kuna haja ya kuwa na mkurunzi wao mbali na mkurugenzi wa afya kwa kaunti nzima na serikali ikifeli kuunda kiti hicho tutatoa mwelekeo wetu baadaye na sio sasa hivi,” aliongeza Keriama.
Matamshi hayo yaliungwa mkono na mwenyekiti wa Kenya national union of nurses Erick Oigo ambaye alisema wauguzi wanastahili kuwa na mkurugenzi wao binafsi katika kaunti hiyo kando na yule wa afya kwa ujumla.