Share news tips with us here at Hivisasa

Ajali kwenye barabara za humu nchini zinaendelea kuongezeka baada ya watu wengine watatu kuaga dunia katika barabara kuu ya Naivasha kuelekea Mai Mahiu katika visa viwili tofauti siku ya Alhamisi asubuhi.

Ajali hizo zilitokea eneo moja karibu na kanisa katoliki la kimisheni kwenye milima ya Mai Mahiu na kuhusisha trela mbili.

Kwenye kisa cha kwanza, dereva mmoja aliyekuwa akisafirisha mchanga wa ujenzi kutoka Mai Mahiu kuelekea Nairobi alishindwa kudhibiti   lori alilokuwa nalo hatua iliyopelekea kubingiria kwa lori hilo kwenye milima hiyo. Dereva huyo aliaga dunia.

Saa chache baadaye gari lingine lililokuwa limebeba pikipiki kuelekea Kakamega kutoka Nairobi lilianguka na kuwaua watu wawili, dereva na taniboi wake huku gari hilo likisababisha msongamano mkubwa wa magari katika barabara hiyo.

Mmoja wa wakazi wa eneo hilo Joseph Njoroge aliyeshuhudia ajali hiyo, amesema kuwa madereva wote wawili waliaga dunia papo hapo huku kondakta aliyekuwa kwenye gari la pili akipata majeraha mabaya lakini baadaye alidhibitishwa kufariki.

"Dereva wa lori la mchanga alishindwa kudhibiti gari na likaanguka na kubingiria mara kadhaa na tulipoenda karibu, tulimwona ameaga dunia. Yule wa lori lilokuwa likibeba pikipiki alikufa papo hapo baada ya lori hilo kuanguka, ilikuwa ikiendeshwa kwa kasi," alidokeza Bw Njoroge.

Afisaa mmoja wa ngazi ya juu wa polisi japo hakutaka kutajwa jina lake, amedhibitisha tukio hilo na kusema kuwa uchunguzi umeanzishwa huku akiwataka madereva kuwa waangalifu barabarani.