Waziri wa maswala ya mambo ya kigeni nchini Amina Mohammed amekashfu vikali kitendo cha kumdhalilisha mjumbe wa bunge la kaunti ya Kirinyaga kilichotekelezwa na vijana wa Malindi wakati wa uchaguzi wa eneo bunge la Malindi.
Akiongea na wanahabari katika hoteli moja mjini Mombasa siku ya Alhamisi baada ya kuhudhuria kongamano la akina mama kuhusu maswala ya wanawake na uongozi, Amina amesema kuwa kitendo hicho kimeonyesha kudharauliwa kwa wanawake pamoja na kushushwa hadhi kama viongozi.
Amina ametaka kuchukuliwa hatua kali za kisheria kwa waliohusika na kitendo hicho kwani kimeonyesha picha mbaya katika maswala ya uongozi wa wanawake katika mataifa ya Magharibi.
"Tulisikitika kuona jinsi akina mama wanavyodhalilishwa kama kitendo cha juzi kule Malindi, kama viongozi tunataka hatua kali zilichukuliwe dhidi ya wahusika ili iwe funzo kwa watu wengine," alisema Amina.
Wakati huo huo, amewataka wanawake nchini kujitosa katika ulingo wa kisiasa kuhakikisha kuwa wanapigania haki zao kidemokrasia sambamba na kufanikisha usawa wa kijinsia katika maswala ya uongozi na jamii kwa jumla.
Kauli ya waziri huyo imejiri baada ya kushuhudiwa kwa vijana wa Malindi kudhalilisha mjumbe mwanamke wa bunge la kaunti ya Kirinyaga kwa kumvua nguo wakati wa uchaguzi mdogo wa Malindi siku ya Jumatatu.
Picha: Waziri wa maswala ya mambo ya kigeni nchini Amina Mohammed. Amekashfu vikali kitendo cha kumdhalilisha mjumbe wa bunge la kaunti ya Kirinyaga. Wardheernews.com