Mwalimu mmoja kutoka Mombasa alipata bahati ya mtende baada ya kushinda jumla ya milioni kumi kwenye droo ya Lotto iliyofanyika siku ya Jumamosi.
Rachel Munyika alipokea habari hiyo baada ya Lotto kufanya droo yake ya 100 kwenye mchezo ambao umekua ukiendelea kote nchini.
Munyika hakuficha furaha yake baada ya kupokea habari hiyo.
"Nina furaha kubwa sana. Kwa sasa kile tu nawezafanya ni kumshukuru Mungu kwa baraka hii,” alisema Munyika.
Mwalimu huyo mwenye umri wa Miaka 34, alisema kuwa atatumia pesa hizo kuanzisha biashara zitakazomwezesha kupata riziki.
"Sikutarajia kushinda pesa nyingi hivi. Azimio langu ni kuanzisha biashara itakayoniwezesha kujikimu kimaisha kwa muda," alisema Munyika.
Munyika, mwenye watoto wawili, aliongeza kuwa anapania kujenga majumba ya kukodisha ambayo alisema kuwa yatakuwa uwekezaji wa maisha.