Viongozi mbalimbali katika kaunti ya Nakuru wameimiminia sifa serikali ya Jubilee kwa miradi yao ya akina mama na vijana ambayo imesaidia pakubwa katika kuimarisha maisha ya vijana hasa katika kaunti ya Nakuru.
Wakiongozwa na waziri wa elimu, vijana na utamaduni wa kaunti ya Nakuru Joseph Tonui, viongozi hao wamefurahia mchango huo wa serikali kuu katika kuboresha maisha ya vijana.
"Tunafurahia sana miradi ya akina mama na vijana pamoja na uwezo fund ambayo imeimarisha maisha ya vijana na akina mama ambao mara nyingi hawawezi kukimu maslahi yao ya kila siku." Tonui alielezea.
Viongozi hao walikuwa wakizungumza siku ya Jumatano jijini Nakuru wakati wa sherehe ya mgawo wa fedha hizo kwa serikali ya kaunti ya Nakuru ambapo kaunti hiyo ilikabidhiwa shilingi milioni 32 kwa mradi wa vijana na akina mama ikiongozwa na waziri wa huduma ya vijana na masuala ya jinsia nchini Cecily Karuki.
Tonui pia amewaomba vijana na akina mama ambao watanufaika na mradi huo kutumia fedha hizo vizuri ili kuboresha maisha yao.
"Tunawarai vijana wote na akina mama ambao watanufaika na mradi huu kutumia fedha hizo ipasavyo ili kuinua kiwango cha maisha yao. Hii pia itawezesha watu wengine kunufaika na mradi huu katika siku zijazo." Tonui aliongezea.
Baadhi ya viongozi waliohudhuria sherehe hiyo ni pamoja na katibu mkuu wa masuala ya jinsia Zeinab Hussein, mwakilishi wa wanawake Nakuru Mary Mbugua, kamishna wa kaunti ya Nakuru Joshua Nkanatha na wawakilishi wa wadi mbalimbali Nakuru.