Wafanyibiashara wa mahindi katika soko la Keroka wameonywa kuwa watachukuliwa hatua kali ikiwa watafumaniwa wakiuzia wakazi mahindi ambayo yako na sumu.
Hii ni baada ya kubainika kuwa kuna mahindi ambayo hutoka nchi jirani ya Tanzania na Uganda ambayo yako na sumu inayotokana na kutokaushwa kikamilifu, huku zaidi ya gunia 10 za mahindi hayo zikichomwa katika soko hilo.
Akizungumza siku ya Alhamisi mjini keroka, afisa wa afya wilayani Masaba kaskazini Thomas Nyang’au alisema kuna mahindi ambayo hutoka nje ya nchi yakiwa na sumu ambayo ni hatari kwa wakazi.
“Naomba kila mfanyibiashara wa mahindi katika soko la Keroka kuwa maakini na kutoleta mahindi yanayotoka nje yakiwa na sumu maana hiyo ni hatari kwa maisha ya watu wanapoyatumia,” alisema Nyang’au.
“Tumechoma baadhi ya gunia za mahindi ambazo zilipatikana zikiwa na sumu. Pia naomba kila mkazi kuwa maakini anaponunua mahindi ili kutonunua sumu ambayo ni hatari zaidi,” aliongeza Nyang’au.