Wakaazi mjini Nakuru wameitaka serikali ihakikishe mizozo ya mashamba kwenye kaunti hiyo isuluhishwe kabla ya uchaguzi mkuu ujao. Wakaazi wanasema mizozo ya mashamba huenda yakaibua machafuko ya kisiasa ambayo yamekuwa yakishuhudia kwenye bonde la ufa wakati wa uchaguzi.
“Eneo hili linajulikana kuhusu mizozo ya mashamba kwa miaka mingi. Kuanzia miaka ya 1992 kumekuwa na mizozo ya mashamba sana. Mizozo hii tunataka itatuliwe kabla ya uchaguzi,” Kimani Wachira alisema.
Wakiongea siku ya Alhamisi, mwanaharakati Wanjau Mburu alisema huenda wanasiasa wakatumia nafasi hiyo kujitafutia umaarufu na hivyo kusababisha ghasia.
"Angalia ilianza Maella, tena hiyo ya Utheri na sasa ni huko Njoro.Unajua tukiangalia siasa za eneo hilo, mambo ya mashamba yamekuwa yakitumiwa kisiasa haswa maeneo ya Molo,” Mburu alisema.
Akiongea kwa njia ya simu, mwanaharakati Abdi Noor aliitaka serikali kutoa suluhu mara moja kwa tatizo hilo.
“Sisi tunaiambia serikali imalize hii mambo mara moja,” Noor alisema.