Wazazi kaunti ya Mombasa wanapongeza kusimamisha kazi kwa maafisa wakuu wa baraza la mitihani nchini KNEC kutokana kukithiri visa vya wizi wa mitihani.
Wazazi hao walisema kuwa hatua hiyo itakuwa funzo kwa wengine wanaopanga kujihusisha na wizi wa mitihani siku za mbeleni.
Wakizungumza na mwanahabari huyu siku ya Ijumaa, mmoja wa wazazi hao Salim Athuman, kutoka eneo la Barsheba alitaka hatua za kisheria kuchukuliwa kwa wakuu wote wa baraza hilo.
Tangazo la kufutwa kwa wakuu hao lilitolewa kwenye kikao cha wanahabari kilichoandaliwa na waziri wa usalama na masuala ya ndani Meja generali Joseph Nkaissery na Waziri wa Elimu Fred Matiang’I siku ya Alhamisi.
Waliofutwa kazi ni pamoja na afisa mkuu mtendaji wa baraza hilo Joseph Kivilu na mwenyekiti wa bodi inayosimamia baraza hilo Kibiru Kinyanjui.
Aliyekuwa naibu chansela wa chuo kikuu cha Nairobi Prof George Magoha ameteuliwa kuwa mwenyekiti mpya wa bodi hiyo na ataanza kufanya kazi mara moja.
Nkaissery amesema hatua zitachukuliwa dhidi ya waliohusika katika udanganyifu huo.